| MISERICORDIA.newsletter   » zapisz się |  

PL | EN | DE | FR | IT | ES | PT | RU   translate by  GoogleTranslate

MT. PAPA YOHANE PAULO II:

Kwa hiyo, leo, hapa katika Hekalu hili, ninataka kuadhimisha tamko rasmi na la dhati la kuukabidhi ulimwengu kwa Huruma ya Mungu. Ninafanya hivyo nikiwa na shauku kubwa moyoni, nikitamani kwamba ujumbe wa Upendo wenye Huruma wa Mungu, uliotangazwa hapa kwa njia ya Sista Faustina, uwafikie wakazi wote wa dunia na kuijaza mioyo yao matumaini. Ujumbe huu na uenee kutoka mahali hapa katika Nchi yetu pendwa nzima na duniani kote. Na itimie ile ahadi yenye kutuwekea wajibu, aliyoitoa Bwana Yesu, kwamba kutoka hapa inapaswa kutoka “cheche itakayoiandaa dunia kwa Ujio wake wa mwisho.” Cheche hii ya neema ya Mungu lazima ichochewe daima. Moto wa Huruma lazima ukabidhiwe kwa dunia. Katika Huruma ya Mungu, dunia itapata amani, na mwanadamu heri! Jukumu hili ninawakabidhi ninyi, Kaka na Dada wapendwa; ninalikabidhi Kanisa la Kraków na la Poland na Wachaji wote wa Huruma ya Mungu, watakaokuwa wanafika hapa kutoka Poland na kutoka dunia nzima. Iweni Mashahidi wa Huruma!

SALA YA MTAKATIFU PAPA YOHANE PAULO II YA KUIAMINISHA DUNIA NA WANADAMU WOTE KWA HURUMA YA MUNGU

Mungu Baba mwenye Huruma,
uliyedhihirisha upendo wako katika Mwanao Yesu Kristo
na kuumimina juu yetu katika Roho Mtakatifu Mfariji,
tunakuaminisha leo hatima ya ulimwengu na ya kila binadamu.
Utuinamie sisi wadhambi, uuponye udhaifu wetu,
uushinde kila uovu,
uwawezeshe wanadamu wote kuonja Huruma yako ili ndani mwako,
ewe Mungu Mmoja katika Nafsi Tatu,
wapate daima chemchemi ya matumaini.
Baba wa milele, kwa ajili ya Mateso Makali na ya Ufufuko wa Mwanao,
utuhurumie sisi na dunia nzima.

aliisali 17/8/2002 siku ya kutabaruku Basilika ya Huruma ya Mungu Łagiewniki-Kraków, Poland